DC MPOGOLO AWATAKA WENYEVITI WA MITAA NA ASKARI KUFANYA KAZI KWA WELEDI KULINDA AMANI


MKUU WA WILAYA YA ILALA MH. EDWARD MPOGOLO

Na Mwandishi Wetu

DAR ES SALAAM

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Mh. Edward Mpogolo amewataka Wenyeviti wa Mitaa na askari polisi wa ngazi ya Kata kuimarisha ushirikiano katika kulinda amani na usalama ndani ya wilaya hiyo.

Wito huo ameutoa leo jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kilichowakutanisha na viongozi hao kuwapa maelekezo.

Dc Mpogolo amesema kuwa usalama wa wananchi unaanzia katika ngazi ya mtaa, hivyo ni wajibu wa viongozi hao kufanya kazi kwa umoja na mshikamano.

“Ulinzi na usalama unaanzia kwenye mtaa, hivyo ushirikiano wenu ndiyo nguzo ya amani ya wilaya yetu,” amesema Mpogolo.

Amewataka viongozi hao kuwa walezi wa vijana, hususan waendesha bodaboda na wamachinga, akisisitiza kuwa ni kundi muhimu katika shughuli za kiuchumi na kijamii za kila siku. Alisema vijana wanahitaji mwongozo na ushirikiano ili wawe chachu ya maendeleo, si chanzo cha hatari.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, alimuhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa miundombinu yote ya serikali iliyoharibiwa baada ya Uchaguzi Mkuu inaendelea kukarabatiwa ili huduma kwa wananchi zirudi katika hali yake ya kawaida. Alibainisha kuwa baadhi ya ofisi za serikali na vituo vya polisi vilipata uharibifu, hali iliyosababisha wananchi kukosa huduma muhimu kwa muda.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Kipolisi Ilala (RPC) Mgonja aliwahimiza wananchi kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu au vitendo vinavyohatarisha usalama katika maeneo yao, akisema taarifa zao ni ngao muhimu katika kulinda amani ya mtaa.

Kikao kazi hicho kililenga kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yote ya Wilaya ya Ilala na kuhakikisha jamii inaendelea kuishi kwa amani na utulivu.


Chapisha Maoni

0 Maoni