VETA YAWAFIKIA WATOTO UJUZI KWA VITENDO

Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA. Antony Kasore, akiwa amekamata tuzo katika banda la VETA


Na Mwandishi Wetu-Nifahamishe News

MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imetenga eneo maalum katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba kwa ajili ya kuwawezesha watoto na vijana kujifunza kwa vitendo kukuza maarifa katika masomo yao.

Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA. Antony Kasore, ameyasema hayo leo Julai 7,2025 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba.

CPA.Kasore amesema hatua hiyo inalenga kuunga mkono utekelezaji wa Sera mpya ya Elimu ya mwaka 2023 iliyoanzishwa rasmi na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambayo imeweka msisitizo katika elimu ya amali kuanzia ngazi ya msingi hadi sekondari.

"Kwa kuzingatia mageuzi ya kisera katika elimu, tumeona ni muhimu kuwajengea watoto msingi wa ujuzi wakiwa katika umri mdogo. Kupitia eneo hili maalum la maonesho, watoto wanapata fursa ya kujifunza kwa vitendo namna ya kutengeneza bidhaa mbalimbali, kusuka nywele, kazi za umeme pamoja na ufundi seremala," amesema 

Amefafanua lengo ni kuwahamasisha watoto, wazazi na jamii kwa ujumla kuhusu nafasi kubwa ya ujuzi wa vitendo katika maendeleo ya taifa na kupunguza utegemezi wa ajira rasmi.

Aidha ametoa wito kwa wahitimu wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu kujiunga na mafunzo ya ufundi VETA ili kupata ujuzi wa kujiendeleza kiuchumi.

Ameeleza kuwa wapo wahitimu wa elimu ya juu waliopata mafunzo ya ufundi na kufanikiwa kujiajiri, huku wengine wakianzisha makampuni yao na kutoa ajira kwa wengine.

“Tunatoa wito kwa vijana waliomaliza vyuo vikuu kutambua kuwa ujuzi ni hazina. Kuna mifano hai ya wasomi waliokuja VETA baada ya shahada zao na sasa ni wamiliki wa viwanda vidogo na waajiri wa wenzao,” amebainisha.

1Maonesho ya Sabasaba mwaka huu yameendelea kuonesha mchango mkubwa wa taasisi za mafunzo kama VETA katika kukuza ujuzi na kuhamasisha ajira kupitia vitendo, sambamba na kuunga mkono jitihada za serikali za kujenga uchumi wa viwanda unaotegemea rasilimali watu wenye stadi stahiki.

Chapisha Maoni

0 Maoni