SEKTA YA BAHARI KICHOCHEO KUKUZA UCHUMI NCHINI


Dar es Salaam,

Pilly Kigome-Nifahamishe News

SEKTA ya Bahari ni mhimili mkubwa wa kukuza uchumi wa Taifa kupitia shughuli za usafirishaji wa mizigo na watu katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Hayo ameyasema Mkurugenzi Mkuu Shirika la Wakala wa Meli Tanzania(TASAC) Mohamed Salum alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari  leo Julai 7, 2025, katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Saba Saba) katika banda hilo.
Salum amesema kuwa sekta hiyo ni sekta muhimu sana katika ukuaji wa uvhumi nchini hivyo ni vyema wakachangamkia sekta hiyo.

“Tunawaalika wananchi na hasa vijana kutembelea Banda la Marine. Hapa watajifunza si tu kuhusu majukumu ya TASAC, bali pia kuhusu mafunzo yanayotolewa kwa mabaharia, fursa za ajira, na nafasi zilizopo katika sekta ya usafirishaji majini,” amesema.

Ameeleza kuwa TASAC ina jukumu la kusimamia shughuli zote za usafiri wa majini, kutoa vyeti vya ubora kwa vyombo vya majini, kufanya ukaguzi wa meli za kimataifa, na kuhakikisha mazingira ya bahari yanabaki salama na safi dhidi ya uchafuzi unaoweza kusababishwa na kumwaga mafuta, kutupa taka au chakula majini.

Vilevile inatoa leseni kwa shughuli za bandari, hufanya tathmini ya maeneo yanayofaa kwa ujenzi wa bandari, na kuweka viwango vya utendaji kwa taasisi kama DP World na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), wakizingatia namna shughuli hizo zinavyoathiri kasi na usalama wa upakiaji na upakuaji wa mizigo.

Pia Mkoa wa Dar es Salaam ni mfano mzuri kwa kuwa na maeneo mengi ya bandari pamoja na vituo vya kuhifadhi makontena (ICDs) nje ya bandari, ambapo TASAC hutoa leseni na kusimamia hata shughuli ndogo kama za clearing and forwarding.

Wakati huohuo amewahamasisha vijana kujikita katika kusomea kozi za ubaharia, akisisitiza kwamba kuna wigo mpana wa ajira za kimataifa ndani ya sekta hiyo.

“Sekta ya bahari imejaa fursa za ajira zisizochoka. Ni wakati wa vijana kuchangamkia mafunzo haya, kwa sababu mchango wao ndio unaohitajika ili kulijenga Taifa lenye uchumi wa buluu,” amesisitiza.

TASAC inaendelea kutoa elimu, hamasa, na maarifa kwa wananchi kuhusu namna sekta ya bahari inavyoweza kuwa kichocheo cha maendeleo endelevu kwa Tanzania.

Chapisha Maoni

0 Maoni