MATUMIZI YA TEKNOLOJIA YA KIDIJITALI YAVUTIA WANANCHI BANDA LA PURA

MHANDISI CHARLES SANGWENI AKIZUNGUMZA NA VYOMBO VYA HABARI


Na Pilly Kigome-Nifahamishe News

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni amesema kuwa maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) mwaka huu yamekuwa ya kipekee kutokana na matumizi makubwa ya teknolojia ya kidijitali na mwamko mkubwa wa wananchi kutembelea banda la PURA.

Ameyasema hayo leo Julai 9,2025 alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere (Sabasaba).

Eng. Sangweni amesema kuwa PURA imekuwa ikishiriki maonesho haya kila mwaka, lakini kwa mwaka huu, mafanikio ni makubwa zaidi.

“Tunaona faraja kuona wananchi wakifika kwa wingi, wakiuliza maswali ya msingi na yenye mantiki kuhusu sekta ya mafuta na gesi. Hii inaonyesha kiwango cha juu cha uelewa unaojengwa kwa jamii kupitia elimu tunayoendelea kuitoa,” alisema.

Amesema miongoni mwa maeneo yanayovutia wageni wengi katika banda hilo ni teknolojia za nishati safi, jambo linaloendana na ajenda ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kuchochea maendeleo endelevu.

“Hii ni ishara kwamba kama taasisi ya umma, tupo sambamba na dira ya serikali kwa kutekeleza kwa vitendo ajenda ya nishati safi na maendeleo jumuishi,” aliongeza Eng. Sangweni.

Akizungumzia majukumu ya PURA, Mhandisi Sangweni amesema kuwa moja ya kazi kuu ya mamlaka hiyo ni kusimamia ushiriki wa Watanzania na makampuni ya ndani katika shughuli za mkondo wa juu wa petroli.

“Wakati PURA inaanzishwa, asilimia 55 ya kazi zilikuwa zikifanywa na makampuni ya wazawa. Hivi sasa, takwimu zinaonyesha ongezeko kubwa hadi kufikia asilimia 85, jambo ambalo ni la kujivunia kwa taifa,” ameeleza.

Aidha amefafanua kuwa kwa sasa kuna kampeni ya uchimbaji visima vya gesi mkoani Mtwara, ambapo visima vitatu vinaendelea kuchimbwa. Katika kazi hiyo, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linashiriki kwa asilimia 40 huku wawekezaji kutoka nje ya nchi wakichangia asilimia 60.

 “Hii ni hatua muhimu ya kukuza ushiriki wa kitaifa, kwani kazi ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania zinapewa kipaumbele,” amesisitiza

Mkurugenzi Sangweni amebainisha kuwa PURA imeweka mkazo katika kuhakikisha kuwa kazi zote zinazoweza kufanywa na wazawa zinapewa makampuni ya kitanzania. 

Kwa sasa, kati ya kila makampuni 10 yanayopewa kazi katika miradi ya mkondo wa juu, makampuni sita ni ya ndani.

“Lengo letu ni kuinua uchumi wa Watanzania na kukuza ujuzi wa ndani kwa muda mrefu,” aliongeza.

Chapisha Maoni

0 Maoni