BAADHI YA WANAWAKE WAKIWA KATIKA DUA MAALUM YA KULIOMBEA TAIFA KATIKA MSIKITI WA MFALME WA SITA BAKWATA

BAADHI YA WAUMINI WA KIISLAMU WANAUME KATIKA DUA YA PAMOJA KULIOMBEA TAIFA


Na Pilly Kigome-Nifahamishe News 

DAR ES SALAAM

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania Ofisi ya Mufti imeandaa dua Maalum ya siku tatu yenye lengo kuliombea Taifa amani kuelekea Uchaguzi Mkuu, kuwaombea viongozi wakuu wa dini ya Kiislamu waliotangulia mbele ya haki.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Mei 9,2025 katika viwanja vya Bakwata Ukty.Dotto Maganga Mratibu na Mkurugenzi na Itifaki Kamati ya Dua ya Kitaifa Ofisi ya Mufti amesema wametenga siku hizo tatu maalum kwa lengo la kujikita kuelekeza maombi kwa MwenyeziMungu pekee nchi iendelee kuwa na amani na mshikamano uliopo.

Amesema waumini wa dini ya kiislamu wana wajibu wakufanya dua iwe kwa makundi au kwa mtu mmoja mmoja kuliombea taifa na viongozi wetu wakuu wa nchi hasa katika kipindi hiki cha kueleka Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Taifa Mantum Mahiza amesema kuwa wanawake ni viongozi wakuu kwa familia na jamiika ujumla hivyo wanawake ni chachu ya kuendelea kudumisha amani, uhuru, mshikamano uliopo nchini.

“Tunawaita wanawake wote wa jiji la Dar es salam waje tuungane wka pamoja tuliombee taifa letu, tuwaombee na viongozi wetu wakuu wa nchi na hasa tujikite kuomba amani kuelekea uchaguzi mkuu”

Awali Mei 8, 2025 dua hiyo ilifunguliwa na kuzinduliwa na Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi na Mufti Mkuu wa Tanzania Zuberi Mbwana huku Mei 9, 2025 dua ilifanywa na wanawake huku ratiba ikihitimishwa Mei 10 dua kubwa la kuliombea taifa itafanyika na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa kufungwa na Rais Samia Suluhu Hasssan.

Katika ufunguzi wa dua hizo Mei 8 Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi amesema dua hizo za kuwaombea viongozi waliotangulia mbele ya haki ni ishara njema ya kuwa ni kama sadaka kwa waumini wenzetu ambapo uislamu umehimiza kufanya hivyo.

“Napenda kutumia fursa hii kuwasihi Watanzania wenzangu tuendelee kudumisha mustakabali mwema wa taifa na mshikamano wetu na kujiepusha na yale yatakayoweza kutugawa”. Alisema Rais Mwinyi