Na Mwandishi Wetu- Nifahamishe News Blog
DAR ES SALAAM
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajia kukutana na kufanya mazungumzo na waandishi wa habari ili kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, msemaji mkuu wa serikali, Gerson Msigwa, alisema kuwa Rais Samia amekubali ombi la waandishi wa habari kutaka kuwa na mkutano wa moja kwa moja na yeye, ili kujadili mustakabali wa tasnia ya habari nchini.
Msigwa alifafanua kuwa Rais Samia amemuagiza kutoa ujumbe kwa waandishi wa habari, akisema kuwa anatambua na kuthamini mchango mkubwa wa waandishi wa habari katika kuleta mabadiliko chanya kwa taifa. Ameongeza kuwa Rais Samia ameahidi kuwa serikali itaendelea kushirikiana na waandishi wa habari katika kukuza na kuboresha tasnia hiyo muhimu kwa maendeleo ya taifa.
Aidha, msemaji huyo alisisitiza kuwa mkutano huo na waandishi wa habari unatarajiwa kufanyika hivi karibuni, ambapo Rais Samia atatoa nafasi kwa waandishi kutoa mawazo yao na kujadili masuala yanayohusu ufanisi wa kazi zao.

0 Maoni