ARV ZIPO WANANCHI ONDOENI SHAKA- MSIGWA

 

MSEMAJI MKUU WA SERIKALI GERSON MSIGWA AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI JIJINI DAR ES SALAAM

 

Na Pilly Kigome


SERIKALI ya Tanzania imetangaza kuwaondoa hofu wananchi wake kuwa hakutakuwa na ukosefu wa dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARV) na kukiri dawa zipo na Serikali haitawaacha wananchi wapoteze maisha hata kama Rais wa Marekani Donald Trump atatekeleza mpango wake wa kusitisha misaada ya hisani kwa nchi za Afrika.


Hayo yamesemwa leo Machi Mosi 2025 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.


Msigwa amesema kuwa, Serikali imejidhatiti kwa kutenga fedha za kutosha ili kununua dawa hizo na kuendelea kuzitoa bure kwa wananchi wanaoishi na virusi vya HIV/AIDS.

"Serikali haitamuacha Mtanzania yeyote afe kwa kukosa dawa hizo kwakuwa kuna shehena ya kutosha ya dawa hizo wananchi wanaoishi na virusi vya HIV/AIDS hawapaswi kuwa na hofu, licha ya mabadiliko yanayoweza kutokea katika msaada wa kigeni” amesisitiza Msigwa.


Msigwa amewahimiza watumiaji wa dawa hizo kuendelea kunywa dawa na kufata kanuni kuendelea na maelekezo kutoka kwa wataalamu wa afya na kuacha papara ya kuwaomba wahudumu wa afya wawape vidonge zaidi ili waweke akiba nyumbani kutokana na hofu ya kukosekana kwa vidonge.


Hivi karibuni wameonekana baadhi ya wagonjwa kuwa na hofu ya juu kutokana na hofu uwepo wa kukosekana kwa dawa hizo na wamekuwa wakiomba kupewa dawa nyingi vituoni ili wahifadhi dawa.


Alisema Serikali ina uwezo wa kugharamia dawa hizo kwa kutumia rasilimali zilizopo, na kwamba ukosefu wa misaada kutoka kwa nchi za Magharibi hakutaleta mtikisiko wowote wa kiuchumi nchini Tanzania.

Wakati huohuo alitoa wito kwa Watanzania kuwa ugonjwa wa ukimwi bado upo na kuwataka kuwa makini na kujihadhari na maambukizi mapya hasa kuwataka vijana kuachana na starehe ambazo zitawaweka katika mashaka ya kupata maambukizi ikiwemo ya kutokutumia kinga.


Chapisha Maoni

0 Maoni