ALIYEKUWA MKUU WA WILAYA UBUNGO HASSAN BOMBOKO AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI MARA BAADA YA KUMALIZA KIKAO NA WENYEVITI WA MTAA
DAR ES SALAAM
Na Pilly Kigome- Nifahamishe News Blog
FEBRUARI Mosi, 2025 Halmashauri ya Ubungo inatarajia kuanza shughuli za biashara zitakazofanyika kwa saa 24 katika maeneo yaliyoanishwa kwa lengo la kukuza Uchumi kwa wafanyabiashara pamoja na kukuza mapato ndani ya Halmashauri hiyo.
Hayo yamebainishwa Januari 24,2025 na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Bomboko alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari majira ya Alasiri kabla ya kuhamishwa kwake kuelekea Wilaya ya Hai.
DC Bomboko amesema amekutanisha Wenyeviti wa Serikali za Mtaa kwa lengo la kuzindua kampeni iliyopewa jina la "Ubungo Usiku kama Mchana" katika kuelekea siku hiyo.
Amesema kampeni hiyo mahususi itaenda sambamba na ile ya Mkoa wa Dar es Salaam ya kuanzwa kwa biashara saa 24 itaenda kuonesha taswira halisi ya Wilaya ya Ubungo ambayo ni ya kimkakati na ni lango la jiji la Dar es Salaam na lina masoko makubwa ya kimkakati ikiwemo Kituo kikubwa cha mabasi yaendayo mikoani na daladala.
Amesema maandalizi ya kuelekea usiku kama mchana umekamilika kwa asilimia 80 ikiwemo tayari imeshahakiki usalama wa mfanyabiashara na mali zake na mazingira rafiki ya ufanyaji kazi usiku ikiwemo wamehakikisha huduma zote mhimu zinaendelea kutolewa kwa saa 24 zikiwemo za afya, huduma za kijamii, kama maji na umeme upatikane kwa uhakika kwa saa 24 lakini pia kuwa na uhakika wa miundombinu kama barabara ziwe zinazofikika katika maeneo yote yatakayofanya biashara usiku.
Ameainisha masoko yatakayofanya biashara usiku ni Soko la Mahakama ya Ndizilililopo (Mabibo), Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli (Mbezi), Kituo cha daladala cha Mbezi mwisho, Soko la Kuchinjia kuku la Shekilango na Manzese Bakharesa, Sinza pamoja na Mlimani City.
Aidha alibainisha maandalizi yakikamilika kwa asilimia zote pia wataweza kulifikia Soko la Mburahati, Msigani Maramba, na Soko la Kwa Beda .
Wakati huohuo alitumia mkutano huo kuwafunda wenyeviti wa Mtaa kampeni hiyo iendane sambamba na utendaji wao pia kuwahudumia wananchi kwa saa 24 kuendana na kasi ya kampeni hiyoikiwemo kwenda na kasi ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Pia aliwataka Wenyeviti hao ambao hawaishi kwenye mitaa yao warudi mara moja kuishi katika mitaa ili waweze kuhudumia wananchi kwa saa 24.
0 Maoni