TAASISI WANANCHI WAHIMIZWA MATUMIZI NISHATI SAFI

MEYA ABDALLAH MTINIKA AKIZUNGUMZA NA WANANCHI KATIKA KILELE CHA WIKI YA NISHATI SAFI ILIYOANDALIWA NA STAMICO

Na Pilly Kigome- Nifahamishe News Blog

DAR ES SALAAM

IFIKAPO mwisho wa mwaka 2024 kila Taasisi inayohudumia watu zaidi ya 100 ni lazima watumie nishati safi ya kupikia ikiwa ni kuondoa nishati chafu kwa matumizi ya binadamu.

Hayo yalisemwa jana na Meya wa Manispaa ya Temeke Abdallah Mtinika kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa katika kilele cha wiki ya matumizi ya Nishati Safi kampeni ya Rafiki Briquettes iliyoandaliwa na Shirika la Madini Tanzania STAMICO.

Mtinika amesema kampeni hiyo imekuja kuondoa na kutokomeza matumizi ya Nishati Chafu ambayo sio rafiki kwa Afya na mazingira kwa wanaotumia nishati hiyo.

Mtinika amewataka Wananchi kuchangamkia fursa na kuiamini nishati hiyo na kuanza kuitumia na kuachana na matumizi yasiyofaa ya Nishati chafu.

Aidha amewapongeza wanawake katika makundi mbalimbali ikiwemo Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na Chama cha Wanawake Tanzania (CHAWATA) na vinginevyo kwa kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye kinara wa Nishati Safi

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dokta. Venance Mwasse amesema nishati safi ya kupikia ya Rafiki Briquettes ni Mkombozi katika mapambano dhidi ya nishati Chafu na kwamba Nishati hiyo ni mkombozi kwa Watanzania.

Amesema Nishati hiyo ambayo ni mkaa unaotokana na makaa ya mawe umefanyiwa utafiti na vyuo vikuu mbalimbali na kubainika kuwa unakidhi mahitaji ya watanzania kwani ni rafiki na bidhaa hiyo ni bei nafuu.

Aidha, aliongeza kuwa STAMICO tayari wamesimika mitambo mikubwa ya kuzalisha mkaa huo kwenye Wilaya za Kisarawe mkoani Pwani na Kyela mkoani Mbeya kunakozalisha makaa ya mawe ambapo uzalishaji kwa sasa umefikia Tani elfu ishirini.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Usimamizi wa Majiko kutoka Jeshi la Magereza mkoa wa Dar es Salaam, Sajenti Yohana Simwenda amesema Nishati Safi ya Kupikia ya Rafiki Briquettes imelisaidia Jeshi hilo kuokoa fedha nyingi ikiwa ni pamoja na kuokoa miti ambayo wangeikata kama kuni za kupikia.

Amesema mkaa huo unauwezo wa kupikia vyakula vingi bila kuongeza mwingine huku akisema Gereza moja lenye watu zaidi ya 1000 wanaweza kupikia kilo 19 kwa vyakula vyote na bado ukabaki.



Chapisha Maoni

0 Maoni