NIPO, NITAKUWEPO NA NITAGOMBEA.ATANGAZA KUTOKUMUOGOPA LISSU


Na Mwandishi Wetu- Nifahamishe News


MWENYEKITI wa CHADEMA, Freeman Mbowe ametangaza rasmi kwamba atagombea tena kwa mara nyingine kwenye Uchaguzi wa Chama hicho ili kutetea kiti chake cha Uenyekiti wa CHADEMA Taifa akichuana na Viongozi wengine ambao wanagombea nafasi hiyo akiwemo Tundu Lissu.

Akiongea na Wahariri Jijini Dar es salaam leo December 21,2024, Mbowe amesema “Nimetafakari kwa kina sana, nimesema mara nyingi nilitamani kuondoka lakini siwezi kuondoka na minyukano ambayo ipo ndani ya Chama , kwahiyo CHADEMA nipo, nitakuwepo, nitagombea na Mimi na Viongozi wenzangu wanaoniunga mkono na wasioniunga mkono naamini tutakutana kwenye mazungumzo tuweke mambo sawa, sijawahi kuzuia Watu kugombea, anayetaka kugombea tukutane kwenye box”

“Wazee walioasisi Chama chetu hawakuondoka madarakani kwakuwa walitaka kung’atuka, waliamua kuondoka kwasababu walikuwa wametimiza wajibu wao mkubwa wa kujenga Chama imara chenye itikadi na sera madhubuti, tukumbuke Mzee Edwin Mtei Mwenyekiti wa kwanza wa Chama aliondoka akiwa na umri wa miaka 68, miaka mitano baadaye Mzee Bob Makani Mwenyekiti wa pili yeye aliondoka akiwa na miaka 67, wote waliondoka sio kwasababu ya kushindwa bali kwakuwa walikuwa wamemaliza kazi zao za kuimarisha sera”


“Nilipokea kijiti cha kuongoza Chama chetu September 14,2004, katika miaka hiyo 20 ni kipindi cha miaka 11 tu ya kwanza ambapo tulifanya kazi kikamilifu ya kujitoa ili kukijenga Chama chetu kuwa Chama makini na tukapiga mafanikio ya kufanya tuwe Chama Kikuu cha Upinzani Tanzania”

“Tumefanya mambo mengi ikiwemo kubuni vazi maarufu la Chama maarufu kama kombati na kuongeza thamani ya Chama chetu kwa kuvuta Wanasiasa makini kutoka Vyama vyote na Vyuoni hadi Watu wakafananisha Chama na Real Madrid ambayo inaweza kuvuta Mastaa kutoka Timu mbalimbali, tukapata wengi Mastaa waliokuja kuongeza thamani ya Chama chetu”

Chapisha Maoni

0 Maoni