Na John Bahati-Pwani
ZAIDI ya watoto 5,000 waliokuwa wanasafirishwa kwenye biashara haramu ya binadamu, utumikishwaji wa kingono na ukatili wa kijinsia, wameokolewa na Kituo cha Makazi Salama cha DMI Spring Hope kilichopo Kibamba jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Kituo cha Mission Afrika DMI, Vijili Dali, kwenye maadhimisho ya kupinga usafirishaji haramu wa binadamu yaliyofanyika ofisi ya kituo hicho.
Amesema katika kipindi cha miaka 20 tangu kuanzishwa kwa kituo hicho zaidi ya watoto 5,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini wameokolewa kwenye mazingira ya utumikishwaji wa kingono ukatili wa kijinsia.
“Miongoni mwa sababu zinazochangia watoto wetu kuingia mikononi mwa watu wasiofaa ni wazazi au walezi kuwatumia kama chanzo cha kipato, wanawalazimika kwenda kufanya kazi ili kupata fedha za kuendesha maisha yao jambo ambalo ni kinyume na sheria ya mtoto na sera za kitaifa na kimataifa zinazohusika na ulinzia na usalama wa mtoto,”amesema
Katika kuhakikisha ulinzi na usalama wa mtoto na kumsaidia kutimiza ndoto zao, vijili amewaasa wazazi kuwalea watoto kwa upendo, kujitahidi kuwatimizia mahitaji yao na kuwa karibu ili kujua mienendo yao.
Akizungumza katika maadhimisho hayo,Ofisa Tarafa wa Wilaya ya Ubungo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Bomboko, amesema inahitajika nguvu kati ya serikali, mashirika na wananchi kuhusu ulinzi na usalama wa watoto ili kukabiliana na wimbi la utoroshaji na ukatili wa watoto unaoripotiwa kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Amesema vitendo vya watoto kutekwa na kuuawa vimeshamiri kwenye jamii ikidaiwa chanzo cha kufanya hivyo ni Imani za kishirikina ili kupata fedha kwa kuua watu.
“Kila mtu anapaswa kuwa mlinzi wa mwenzake na muhimu tuache kumuamini mtu yeyote hata kama ni ndugu dunia ya sasa imejaa watu wasio wema,baadhi wanatamaa ya mali wako radhi kuua ndugu zao, tupendane na tulindane,”amesema Beatrice.
0 Maoni