Na Pilly Kigome-Nifahamishe News Blog
DAR ES SALAAM
CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimetoa wito kwa vijana nchini kuchangamkia fursa kozi mpya za kimkakati kuendana na soko kubwa la ajira ndani na nje ya nchi.
Afisa Uhusiano wa NIT, Juma Manday ameyasema hayo katika banda la chuo hicho katika Maonesho ya 48 ya Biashara Kimataifa Sabasaba jijini Dar es Salaam.
Amefafanua kozi nne za kimkakati ambazo kwasasa ndizo kozi ambazo zinauhitaji wa wataalamu ikiwemo kozi wahandishi wa ndege, kujenga na kukarabati meli, wataalam wa mafuta na gesi na wataalam wa kusimamia shughuli za bandari.
Amesema kozi hizo za kimkakati Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Rais Dkt. Samia Sluhu Hassan imezipa kipaumbele katika mwaka wa masomo wa 2024/25 utakaoanza Oktoba mwaka huu.
“Wanafunzi hawa wamepewa kipaumbele kikubwa sansa na Serikali hata wanapoanza masomo katika ngazi stashahada wanapewa mkopo hadi watakapomaliza masomo yao” amesema
Serikali ina mikakati mikubwa katika kulijenga Taifa ikiwa na pamoja kuwa na mikakati la kulifufua Shirika la ndege, kujenga viwanja vya ndege na kuvipanua hivyo kutakuwa na ukubwa wa kuhitaji wataalamu kwa wingi.
Aidha amesema kupitia kozi hizo vijana wataweza kupata utaalamu wa kutosha unaoendana na uhitaji wa wataalamu pamoja na kuweza kujipatia ajira zinazoendana na soko.
“Katika maonesho haya tunaendelea kutoa elimu kwa wanafunzi, wazazi katika kuzitambua kozi hizi na zingine nyingi ambazo zinapatikana NIT” amesema
Mbali na hilo pia ametoa wito kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne na cha sita kuomba kozi hizo ili waweze kusomea masomo hayo.

0 Maoni