MHASIBU MBARALI MBEYA KITANZINI

 


Na Mwandishi Wetu-Nifahamishe News

MBEYA

MAHAKAMA ya Wilaya Mbarali imemhukumu aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Bw. Joseph Werema Ndimila adhabu ya kulipa faini ya Tsh. 1,100,000/= au kwenda Jela mwaka mmoja na kuamriwa kurejesha kiasi cha sh. 4,000,000/= alichokifanyia ubadhilifu baada ya kukutwa na hatia.

Werema alikutwa na hatia katika makosa ya kutumia nyaraka kwa lengo la Kumdangaya Mwajiri, Kutumia Vibaya Madaraka na kosa la Kufanya ubadhilifu ambayo ni kinyume na vifungu vya 22, 31 na 28 vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa [CAP 329 R.E 2022].

Hukumu dhidi ya Bw. Ndimila imetolewa Julai 26, 2024 kutokana na shauri la Uhujumu Uchumi Na. 18/2023 lililokuwa katika Mahakama ya Wilaya Mbarali mbele ya Hakimu Mkazi Aliko Michael Mwandumbya, shauri ambalo liliendeshwa na Mwendesha Mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bw. Sospeter Tyeah.

Imeelezwa kuwa Mshtakiwa alifikishwa mahakamani kwa mashtaka tajwa hapo juu kwa kuandaa nyaraka za uongo za malipo (pay lists) akionesha kuwa aliwalipa watu mbalimbali kwa kukodi kumbi kwa ajili ya kufanya semina katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na kulipa Jumla ya sh. 4,000,000/= huku akijua kuwa malipo hayo ni ya uongo na alilenga kumdanganya mwajiri wake na kujipatia kiasi cha sh. 4,000,0000/=

Aidha Bw. Ndimila amelipa faini yote ya sh. 1,100,000/= na amerejesha kiasi chote cha sh. 4,000,000/= alichokifanyia ubadhirifu.

Chapisha Maoni

0 Maoni