MAFURIKO ABIRIA SGR SAFARI DAR-DODOMA



DAR ES SALAAM

Pilly Kigome-Nifamishe News

MAFURIKO ya abiria yameibuka katika safari ya kwanza ya treni ya mwendokasi SGR kutoka Dar es salaam kwenda Dodoma na kupelekea baadhi ya abiria kushindwa kusafiri kwa kukosa nafasi kutokana uwingi wa abiria mabehewa yote kujaa.

Mkurugenzi wa TRC Masanja Kadogosa akizungumza na vyombo vya habari

Hayo yamesema leo Julai 25 na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari majira ya saa 11.19 alfajiri katika kituo kikuu cha abiria SGR cha jijini Dar es salaam.

Kadogosa amesema kuwa mabehewa yote 14 yaliyofungwa kubeba abiria kwa safari hiyo yalijaa huku wengine wakikosa nafasi ya kusafiri kutokana na uwingi wa abiria.

Amesema kutokana na muitikio huo hata kama wangeweza kufunga mabehewa 20 wanaamini yote yangeweza kujaa kutokana na hamu ya watanzania wengi kusafiri kwa kutumia usafiri huo na kusave muda.

Amesema kwa safari hiyo ya awali zaidi ya abiria 1000 wameweza kusafiri kutumia usafiri huo na hakuna siti ambayo ilisalia bila kukaliwa na abiria kwa madaraja yote.

“Tunamshukuru Mungu safari ya kwanza tumeianza leo Julai 25, tumeweza kusafiri na baadhi ya viongozi wakiwemo wakurugenzi, wabunge na baadhi ya wajumbe wa bodi kwa kutumia usafiri huu” amesema

Mbali na hilo Kadogosa amesema wanamshukuru Mungu kwa kuweza kutimiza maelekezo na maagizo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza kuanza kwa usafiri huo kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma kabla kuisha kwa mwezi Julai.

Ikiwemo kumshukuru Rais kwa juhudi zake kubwa kwa kuwauliza kila hatua na kuwauliza changamoto walizokuwa wanakabiliana nazo katika kuanza safari hiyo ikiwa na kuwauliza mara kwa mara nini wanahitaji kutoka kwake inimradi safari hiyo ianze.

Aidha amefafanua usafiri huo utazinduliwa rasmi na Rais Samia Suluhu Hassan ndani ya wiki hizi mbili.

Baadhi ya abiria waliyozungumza na Mtandao huu waliokuwa wakitegemea kusafiri na treni hiyo akiwemo Rose Mchau mkazi wa jijini Dar es Salaam amesema anayofuraha sana kwa kuanza kwa usafiri huo kwa kuwa yeye ni mwenyezi wa Mkoani Dodoma hivyo amefanya juu chini safari ya kwanza awepo ili kuoanisha kati ya basi na treni.

“Kwanza nimevutiwa sana na kutumia masaa machache ya kusafiri ,pili nimependa mazingira ni masafi sana kama tuko Airport, hivyo nitawahimiza watu wa Dodoma wenzangu waje kwawingi kutumia usafiri huu na sio uzushi kama tulivyojua awali” amesema

Mohamed Makongoro mkazi wa Tabata anaelekea Dodoma amepata tenda ya shughuli zake za uchukuaji picha(cameraman) ameona atumie usafiri huo ili kuendana na muda kuliko kutumia usafiri wa basi.

“Tumpe hongera sana mama (Rais) mama ameweza kutukamilishia usafiri huu nimefurahi sana sana kwani usafiri huu umekuja kuimarisha uchumi kwa sisi watu wenye uchumi wa chini na kati tutafanya biashara na mambo yetu kwa wakati” amesema

Treni hiyo ilitoka Dar es Salaam majira ya saa 12 kamili asubuhi na kufika mkoani Dodoma majira ya saa 3.30 asubuhi.

Usafiri huo unakwenda na muda bila kujali kuna abiria wangapi hawajaingia kwenye usafiri kwani Mtandao huu ulishuhudia baadhi ya abiria waliochelewa dakika 2 kuingia kwenye mabehewa ilishindikana kusaidiwa kwani dakika tano kabla kuanza kwa safari mabehewa yanafungwa katika mfumo uliowekwa.




 

Chapisha Maoni

0 Maoni