BASHUNGWA AIAGIZA TBA KUSHUGHULIKA NA WADAIWA SUGU,ATAKA WAPANGAJI KULIPA KODI KWA WAKATI


Na Mwandishi Wetu-Nifahamishe News Blog

DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewataka wapangaji wanaoishi katika nyumba za Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kulipa kodi ya pango kwa wakai ili fedha hizo zitumike kujenga majengo mapya na kuboresha huduma katika majengo mengine.

Bashungwa ametoa agizo hilo leo Julai 23, 2024 katika hafla ya ufunguzi wa jengo la makazi ya watumishi wa Umma lililopo Magomeni Kota la ghorofa saba katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mkoani Dar es Salaam.

“Serikali itaendelea kufanya kila jitihada za kujenga makazi bora ya watumishi lakini watumishi mliopata fursa ya kukaa kwenye nyumba za TBA, kulipa kodi ni wajibu. Mkilipa kodi inatupa uwezo wa kuboresha huduma ya makazi bora”, amesisitiza Bashungwa.

Bashungwa ameielekeza TBA kusimamia ukusanyaji wa madeni kwa wadaiwa sugu kulingana mikataba waliyojiwekea ili kodi hizo ziweze kukamilisha ujenzi wa jengo la tatu na nne (Block C na D) yanayoendelea katika eneo la Magomeni ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 15.

Aidha, amesema Serikali imerekebisha Sheria za TBA na kutoa fursa kwa kuingia ubia na sekta binafsi ili kurahisisha ushirikishwaji wa Sekta Binafsi na Taasisi za fedha kwa ajili ya uendelezaji wa milki, kuwahudumia watumishi wa umma wenye uhitaji wa makazi.

Bashungwa ameeleza kuwa ujenzi wa jengo la makazi ya watumishi wa umma la Magomeni Kota Awamu ya Pili B lililogharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 5.6 ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020 - 2025 na ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha Makazi bora.

Kadhalika, Bashungwa ameipongeza TBA kwa matumizi bora ya ardhi na mipango mizuri ya majengo ya kisasa katika eneo la Magomeni lenye ekari 32,000 lililokuwa na wakazi zaidi ya 645 kwa kuweza kutumia ekari 9 kutosheleza wakazi hao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameeleza kuwa Mkoa huo unatakiwa kupangwa upya kwa kuwa na mikakati ya pamoja kwa kushirikiana na Mashirika ya Kiserikali na Sekta Binafsi ili kuuwezesha Mkoa huo kuwa miongoni mwa miji mikubwa Afrika kufikia mwaka 2030.

Akitoa taarifa ya mradi, Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro ameeleza kuwa kazi zote katika mradi huo za ubunifu, ujenzi na usimamizi zimetekelezwa na TBA kwa kutumia Wataalam wake wenyewe kwa kuzingatia mabadiliko chanya ya ukuaji katika Sekta ya Uchumi, Mipango Miji na Teknolojia ya Ujenzi, Mawasiliano na Miundombinu.

Kondoro ameeleza kuwa jengo hilo limefungwa mfumo wa kisasa wa ‘Payless’ ambapo itakapofika wakati wa kulipa kodi ya pango na mpangaji akawa hajalipa, moja kwa moja anakosa huduma ya umeme na maji katika nyumba yake na akilipa kodi ya pango, muda huo huo huduma ya umeme na maji inarejea.




 

Chapisha Maoni

0 Maoni