TAASISI YA MAMA ONGEA NA MWANAO YAWAFIKIA WATOTO WENYE ULEMAVU KWA KUWAPATIA VITI MWENDO

STEVE NYERERE AKIZUNGUMZA NA VYOMBO VYA HABARI JIJINI DAR ES SALAAM


DAR ES SALAAM

Na Pilly Kigome

TAASISI ya Mama Ongea na Mwanao kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wamewapatia watoto wenye ulemavu viti mwendo (Baiskeli) 250 ili kuweza kutimiza ndoto zao za kielimu na urahisi wa mahitaji mengine ya kijamii.

Akizungumza na vyombo vya habari Juni 11,2024 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Steve Nyerere amesema wamewiwa kutoa msaada huo kwa watoto wenye uhitaji maalum  kwakuwa baadhi ya wazazi wamekuwa wakipitia nyakati ngumu kuwahudumia watoto hao.

Amefafanua mara nyingi wazazi hao hasa wanawake wamekuwa wakikimbiwa na wenziwao baada ya kujifungua kwa kupata watoto wa aina hiyo.

“Kupata mtoto mwenye changamoto ya ulemavu hakuna anayependa  ni mipango ya Mungu na sio mikosi wala nuksi hivyo jamii tuache fikra potofu”

Kwa upande wake Katibu wa Taasisi hiyo Evon Cherry amesema taasisi hiyo imetembelea mikoa mitano kutoa misaada mbalimbali ikiwemo ya kuwavisha watoto viatu na sasa wamebakisha mikoa miwili kumaliza na kuwafikiwa wote.

"Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anawasaidia wakina mama katika sekta ya Afya,Maji lakini Sisi tumeamua kumtua mama mtoto mgongoni" amesema Evon

Chapisha Maoni

0 Maoni