Na Pilly Kigome-Nifahamishe News
DAR ES SALAAM
VIFO vitokanavyo na uzazi vimepungua kutoka 556 kwa vizazi hai 100,000 mwaka 2015/16 hadi kufikia 104 mwaka 2022.
Mbali na hilo vifo vya watoto wachanga bado viko juu kutoka vifo 25 kwa vizazi hai 1,000 mwaka 2015/16 hadi 24 kwa vizazi hai 1,000 mwaka 2021/22.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu Jijini Dar es Salaam katika matembezi ya kuanzisha uchangiaji wa mfuko wa ujenzi wa kituo mahususi kwa ajili ya wanawake na watoto yaliyofanywa na Chama Cha Madaktari Wanawake Tanzania(MEWATA).
Waziri Ummy amesema vifo hivyo vya watoto wachanga ni sawa na wastani wa watoto 50,000 kwa mwaka sawa na vifo 140 kwa siku.
Amefafanua takwimu hizo ni baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kupokea ripoti ya utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto ya mwaka 2021/22 TDHS.
Rais wa MEWATA Dkt. Zaitùni Bokhary amesema ujenzi wa kituo hicho umelenga kuendelea kujikita kupambana na magonjwa yanayoshambulia wanawake saratani kwa asilimia kubwa yakiwemo saratani ya mlango wa kizazi, saratani ya matiti
Ikiwemo kukuza mshikamano na uhusiano kuhimiza na kukuza utafiti na kuboresha afya kwa wanawake na watoto huku kutetea mabadiliko ya sera katika sekta ya afya.
Dkt.Bokhary amesema lengo la kuanzisha kituo hicho ni kuweka mazingira salama ya wanawake kupokea huduma kamili za afya, elimu na usaidizi unaoendana na mahitaji ya mahususi.
Amefafanua tayari wameshaanza kufanya mazoezi ya kupima afya za akina mama katika mikoa mbalimbali ikiwemo Mbeya,Njombe, Tabora, Manyara, Dodoma, Mtwara, Lindi, Songea na Mwanza.
Katika mazoezi hayo wamefanikiwa kuwafikia kuwafanyia uchunguzi wa awali wa saratani ya matiti akina 73,744 na uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi akina mama 9,307.



0 Maoni