Na Pilly Kigome
DAR ES SALAAM
JUKUMU la malezi ya watoto si kwa mzazi pekee bali na kwa jamii iliyowazunguka ili kuweza kutengeneza Taifa imara na bora lisilokuwa na mmomonyoko wa maadili.
Rai hiyo imetolewa April 6 Jijini Dar es Salaam na Diwani wa Kata ya Buguruni Busoro Pazi katika mashindano ya msimu wa Pili wa kusoma kuruani katika kata hiyo yaliyofanyika katika Shule ya Msingi Buguruni.
Pazi amesema lengo la kuanzisha mashindano hayo ni kuhamasisha usomaji, uhifadhi kuruan ikiwemo na kukuza maadili kwa watoto wadogo katika kata hiyo.
“Ni jukumu la kila mmoja kuwalinda watoto wetu katika suala zima la maadili, mimi kama kiongozi nina wajibu wa kuwakuza watoto wetu kuwaweka karibu na Mungu ili kuondoa ama kupunguza mmomonyoko wa maadili ambao sasa umekithiri” amesema Pazi
Mbali na hilo Pazi alitilia mkazo kwa kauli mbiu ya mashindano hayo kwa kumnukuu Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Hayati Ali Hassan Mwinyi kwa kusema”Maisha ya mwanadamu ni hadithi tu hapa ulimwenguni, jitahidi kuwa hadithi nzuri kwa hao watakaosimuliwa”
Aidha aliweza kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea zaidi ya Bil.7 katika kata hiyo kuleta maendeleo na fedha za ruzuku Mil 90 wameshaanza ukarabati wa vyumba sita vya madarasa ikiwemo na miradi mbalimbali ya maendeleo hususani ya elimu.
Shekhe wa Wilaya ya Ilala, Adam Mwinyipingu amesema wataunga mkono juhudi alizoanzisha diwani Pazi na kuhamasisha zaidi jamii kuhusiana na elimu na umuhimu wa dini.
SHEKHE WA WILAYA YA ILALA ADAM MWINYIPINGUKatika mashindano hayo jumla ya watoto 38 walishiriki katika mashindano hayo ambapo walishindanishwa makundi matano likiwemo waliosoma juzuu 1, juzuu 2, juzuu 3, juzuu 5 na juzuu 7.
Mshindi wa kwanza katika Juzuu 5 ni Saada Rashid aliyepata point 98 alijinyakulia zawadi ya redio yenye Spika tatu na TV ya inchi 21.
Mshindi wa jumla katika mashindano hayo wa juzuu 7 alikua ni Shureh Khatibu Kombo aliyetokea Madrasat Daarul Quruan mtaa wa Madenge aliweza kujinyakulia zawadi ya Jokofu.
Washindi wengine katikakila kundi waliweza kujipata zawadi mbalimbali ikiwemo madaftari, pasi za umeme, mafeni, majiko ya gesi na visagio (Brenda)






0 Maoni