Na Mwandishi Wetu
MASASI
WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameelekeza Wakala wa Barabara (TANROADS) kuhakikisha wanarejesha mawasiliano ya barabara iliyokatika eneo la Maili Mbili katika barabara ya Mtwara-Mingoyo-Masasi ndani ya masaa matatu mara baada ya Daraja kusombwa na maji.
Bashungwa ametoa agizo hilo leo Machi 04 Wilayani Masasi akiwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Deo Ndejembi, walipofika kutembelea kujionea adha ya watumiaji wa barabara hiyo.
Abiria wanaotumia njia hiyo wamedaiwa kukwama kwa masaa kadhaa kutokana na kukatika kwa miundombinu iliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha usiku wa jana.
“Nitoe pole kwa wananchi ambao mmepata changamoto kutokana na kukatika kwa mawasiliano ya barabara inayotoka mkoa wa Ruvuma kuelekea mkoa wa Mtwara na Lindi, Natoa saa tatu kwa TANROADS kuhakikisha inakamilisha kujenga barabara ya mbadala ili magari na wananchi waanze kupita", amesisitiza Bashungwa.
Bashungwa ameeleza kuwa tayari Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa fedha za kumtafuta Mkandarasi atakayeijenga upya barabara hiyo ya Mtwara-Mingoyo-Masasi (km 200) kwa kiwango cha lami kwa kuwa barabara hiyo imekwisha muda wake na imechakaa.
“Wizara ya Ujenzi tumeshapokea maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan hadi kufikia Mwezi wa Sita Mkandarasi awe ameshapatikana na kuanza kazi ya kuijenga upya barabara hii”, amefafanua Bashungwa.
Naye, Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Deo Ndejembi ameeleza kuwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa kiasi cha Shilingi Bilioni 30 kwa ajili ya dharura za matengenezo ya barabara nchi nzima kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) na hivyo wamejipanga vyema kutatua changamoto zozote za mawasiliano ya barabara pindi zinapotokea.
Kwa upande wake Mbunge wa Masasi, Geofrey Mwambe, ameishukuru Serikali na timu nzima ya watalaam wa TANROADS kwa kuchukua hatua za haraka za kuhakikisha wanaanza kazi ya kurejesha mawasiliano ya barabara hiyo na miundombinu mingine ambayo imeathiriwa na mvua katika Wilaya ya Masasi.
0 Maoni