TADB YAZIDI KUWANG'ARISHA WAKULIMA NA WAVUVI KWA KUWAWEZESHA MIKOPO

Mkurugenzi wa Benki ya TADB, Frank Nyabundege (kushoto) na Mkurugenzi wa Benki ya TCB, Adam Mihayo wakisaini mkataba wa ushirikiano wa kutoa dhamana ya mikopo ya kilimo, Dar es Salaam jana. Waliosimama ni Mkuu wa Kitengo cha Sheria TADB, Dk. Edson Rwechungura na Mkurugenzi wa Sheria TCB, Mystica Ngongi

DAR ES SALAAM

Na Pilly Kigome

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kupitia Mfuko wake wa Dhamana wa Wakulima Wadogo (SCGS) imefikia makubaliano ya kuongeza mkataba wa ushirikiano na Benki ya Biashara Tanzania (TCB) kwaajili ya kutoa dhamana ya mikopo ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Mkataba huo ulioingiwa kati ya pande hizo mbili utaiwezesha TADB kuchagiza upatikanaji wa mitaji kwa wakulima kupitia TCB ambapo watatoa mikopo kwenye mnyororo wa wa thamani wa kilimo, mifugo na uvuvi na TADB itatoa dhamana ya hadi asilimia 70 kwa mikopo yote hususani kwa vijana, wanawake na miradi inayosaidia kupunguza au kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Mkurugenzi Mwendeshaji TADB, Frank Nyabundege akizungumza mbele ya vyombo vya habari alisema, mkataba huo utaiwezesha TCB kuongeza wigo wa utoaji mikopo katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi hasa kwa wanawake na vijana. 

“Nawapongeza kwakuona umuhimu wa kuendelea kutoa mikopo kwenye sekta za kilimo, mifugo na uvuvi naamini mkataba huu mpya baina yetu, utasaidia kuongeza wigo wa upatikanaji wa mikopo kwa wakulima wadogo na itakuwa rahisi kuwafikia kwa wingi zaidi hususani wale waliopo pembezoni mwa miji, mikoa na wilaya.” amesema 

Amesema ushirikiano kati ya TADB na TCB ulioanza Mei 2018 TCB kupitia dhamana ya TADB ilishatoa mikopo yenye jumla ya Shilingi. Bilioni 34.1 kwa wanufaika wa moja kwa moja 2,638 na wanufaika wasio wa moja kwa moja zaidi ya 7,750.

Amefafanua zaidi ya asilimia 95 ya wanufaika hao ni wakulima wadogo na wajasiriamali wadogo wa vijijini wanaoshughulika na myororo wa thamani wa kilimo, mifugo na uvuvi.

Aidha jumla ya Shilingi bilioni 4.3 zimetolewa kwa wanawake 448 na Shilingi bilioni 3.4 zimetolewa kwa vijana 416 katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini.

Ameongeza kwa kusema kuwa TCB kupitia mfuko wa dhamana wameshafikia jumla ya vikundi na vyama vya ushirika 94 vyenye jumla ya wanachama 2,277. Ili kuongeza wigo kwa TCB kutoa mikopo zaidi, TADB imefanya maboresho na imeongeza kiwango cha dhamana kutoka asilimia 50 mpaka asilimia 70 kwa miradi ya wanawake, vijana na miradi inayosaidia kupungunza au kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi. Hii itaongeza upatikanaji wa mikopo kwa wanawake na vijana na kuchochea ongezeko la ajira nyingi.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa TCB Adam Mihayo, amesema wamefikia uwamuzi wa kuongeza mkataba na TADB kutokana na faida walizozipata kupitia mkataba wa awali.Nakuongeza kuwa kupitia mkataba huo, TCB itaongeza wigo wa kutoa mikopo na kuwafikia wakulima wengi zaidi katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuwapatia mitaji itakayo wawezesha kutoka katika kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha kibiashara kwa riba nafuu zaidi hivyo kumnufaisha mkulima na kuinua uchumi wa nchi kwa ujumla

“Tunaishukuru TADB kwa kutuongezea nguvu kwa ajili ya kuwafikia wakulima, wafugaji na wavuvi wengi zaidi na Mikopo hii inapatikana katika matawi yote ya TCB yaliyopo Tanzania” amesema

Ushirikiano na TCB unafanya jumla ya taasisi za kifedha zinazonufaika na Mfuko wa Dhamana wa Wakulima Wadogo (SCGS) kufika 16. Taasisi hizo zinajumuisha Benki za Biashara, Benki za Kijamii na Taasisi ndogo za fedha (Microfinance Financial Institutions) zenye uwezo wakuhudumia wakulima kupitia mtandao wao wa matawi zaidi ya 700 kote nchini.

Hadi kufikia mwezi Desemba, 2023 jumla ya mikopo iliyodhaminiwa na TADB kupitia mfuko wa SCGS ilikuwa Shilingi bilioni 250.77 kwa wanufaika wa moja kwa moja zaidi ya 19,400 na wanufaika wasio wa moja kwa moja zaidi ya 897,900 kutoka mikoa 27 (87% ya Mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani) na Wilaya 129 (83% ya Wilaya zote Tanzania Bara na Visiwani) ambapo zaidi ya asilimia 95 ya wanufaikaji wote ni wakulima, wafugaji na wavuvi wadogo.

Chapisha Maoni

0 Maoni