MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM ALBERT CHALAMILA AKIONGEA NA VYOMBO VYA HABARI LEO OFISINI KWAKE
DAR ES SALAAM
Na Pilly Kigome
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila ametangaza kuahirisha ziara yake ya kukagua na kusikiliza kero za wananchi katika Wilaya kutokana na msiba wa kitaifa wa Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowasa.
Chalamila alitangaza hilo leo Februari 12 ofisini kwake na kusema ameahirisha ziara hiyo iliyopangwa kuanza leo Wilaya ya Temeke.
Amesema amefanya hivyo ili kuungana na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, familia na Watanzania wote katika msiba huu mzito wa kitaifa.
Amefafanua kutokana na msiba huo kuwa upo mkoani humo basi anatumia muda mwi gi kujipanga vizuri katika nyanja zote ikiwemo Usalama na uratibu wa wageni mbalimbali kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu ambaye ndiye mratibu mkuu wa msiba huo.
Aidha RC Chalamila amesema siku ya kesho Februari 13, mwili wa marehemu Edward Lowassa utaagwa katika viwanja vya karimjee Ilala ambapo ametoa rai kwa wakazi wa Mkoa huo na Watanzania kwa ujumla kutumia siku hiyo kuja kwa wingi kumuaga mpendwa wao, kiongozi wao na Mzee wao huyo.
Vilevile Februari 14, 2024 mwili utapelekwa katika kanisa la Azania Front kwa ajili ya Ibada, na Februari 15, 2024 mwili wa marehemu utasafirishwa kuelekea nyumbani kwao Monduli mkoani Arusha ambapo maziko yanatarajiwa kufanyika Februari 17, 2024 ambayo yataongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MAREHEMU EDWARD NGOYAI LOWASSA ENZI ZA UHAI WAKESambamba na hilo RC Chalamila ametangaza tarehe ya kuanza ziara yake ambapo amesema ziara hiyo itaanza rasmi Februari 19, 2024 Wilaya ya Temeke Jimbo la Mbagala, Februari 20 Jimbo la Kinondoni, Februari 21 Jimbo la Kawe, Februari 22 Jimbo la Kinondoni, Wilaya ya Ubungo.
Februari 23 ziara itaendelea katika Jimbo la Ubungo, Februari 24 Jimbo la Kibamba, Februari 26 na 27 Wilaya ya Kigamboni na Februari 28 Wilaya ya Ilala, Februari 29 Jimbo la Ukongo na kuhitimisha Machi 1 katika Jimbo la Segerea


0 Maoni