HAKUNA NDEGE ILIYOUNGUA NI HITILAFU NDOGO TU-ATCL

MKURUGENZI MKUU WA ATCL MHANDISI LADSLAUS MATINDI AKIZUNGUMZA NA VYOMBO VYA HABARI JIJINI DAR ES SALAAM


Na Pilly Kigome

DAR ES SALAAM

SHIRIKA la ndege la Tanzania(ATCL) limesema tukio lililotokea Februari 24 mwaka huu katika ndege yake aina ya Airbus A220-300 ilikuwa ni hitilafu ndogo ya moja ya injini zake na si kuwaka moto kwa ndege

Hayo yamesema Februari 29 mwaka huu na Mkurugenzi Mkuu wa ATCL Mhandisi Ladslaus Matindi wakati alipokuwa akizungmza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam.

Mhandisi Matindi amesema hakukuwa na tukio lolote la kuwaka moto kwa ndege siku hiyo kulijitokeza kwa hitilafu ndogo katika injini.

Amesema ndege hiyo yenye  namba 106 iliyokuwa tayari imeanza safari kuelekea mkoani Mbeya ililazimika kukatisha safari na kurejea Uwanja wa Ndege Julius Nyerere jijini Dar es Salaam baada ya injini hiyo kupata hitilafu na kusababisha moshi ndani ya ndege.

“Injini ilipata joto sana ndipo moshi ulianza na uliendelea kwa takribani dk 5 tu na baadae tulizima injini moja, matatizo haya yanatokea sana kwa vyombo vya moto ikiwemo ndege kwa wanaoelewa ni kawaida, haikufika mbali ilisafiri kama dk 30 tu na kurudishwa Dar es Salaam ilifika mbuga ya Taifa ya wanyama ya Mikumi na iligeuka” amefafanua

Hata hivyo amebainisha kuwa hali ndani ya ndege ilikuwa ni ya kawaida haikuwa ya kutisha na marubani na wahudumu walichukua hatua za kiusalama kwa kuwapa taarifa abiria kuwa watulivu na kuwatoa hofu wasiwe na wasiwasi.

Mbali na hilo aliviomba na kuvikanya baadhi ya vyombo vya habari kuacha kupotosha jamii kwa kutangaza jambo ambalo si kweli

Hata hivyo ndege hiyo iliporudi Dar es Salaam abiria walibadilishiwa ndege nyingine na abiria 104 waliendelea na safari na 18 waliahirisha safari na kuomba wabadilishiwe tarehe ya safari.

Chapisha Maoni

0 Maoni