ZUNGU AWAFUNDA WANAWAKE GEREZANI

Naibu Spika Mussa Azzan Zungu akisisitiza jambo wakati akizungumza katika jukwaa hilo


DAR ES SALAAM

Na Pilly Kigome

NAIBU SPIKA Jamhuri wa Muungano wa Tanzania (MB) Ilala, Mussa Azzan Zungu amewataka wanawake waachane na mambo ya anasa yasiyo ya lazima na kuwataka waangalie mambo yenye tija yatakayoweza kuwaletea maendeleo ya kiuchumi.

Hayo ameyasema leo Desemba 12 katika uzinduzi wa Uhuishaji wa Jukwaa la Wanawake Kata ya Gerezani lililofanyika katika ukumbi wa Ramgharia jijini Dar es Salaam.

Zungu amewataka wanawake kutoka kata hiyo kulitumia vyema jukwaa hilo kwa mambo ya msingi katika kuhakikisha wanajiletea maendeleo na kuondokana na umasikini ambao hauna ulazima.

Amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeanzisha majukwaa hayo ili kuweza kuwakomboa wanawake kiuchumi na kuondoka na umasikini.

Mbali na hilo amewataka wanawake kutoka kata hiyo kupendana, kuacha unafiki wa maneno madogomadogo, washikamane, wapendane wajidhatiti pia kufikia malengo ya mabadiliko ya kiuchumi.

“Naomba niseme ukweli achaneni na anasa ambazo hazina ulazima, kununua simu ya mkononi za gharama kubwa hayo hayana maana nduguzangu, achaneni pia na utoto wa mjini, kila mmoja atafute biashara ya kufanya ili kufikia lengo” amekanya

Kwaupande wake Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Jamila Simba ameviambia vyombo vya habari kuwa watafanyia kazi maagizo yaliyotolewa na NaibuSpika kwa kuendelea kutoa elimu ya biashara ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazowakabili wanawake katika biashara.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Kata ya Gerezani Bi.Jamila Simba akizungumza wakati wa uzinduzi huo

Diwani wa Kata ya Gerezani Fatuma Abubakari ameviambia vyombo vya habari kuwa, watalitumia jukwaa hilo vyema ili waweze kufikia lengo la majukwaa hayo yaliyoanzishwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

“Kwa nafasi yangu nitajitahidi kuendelea kuwapa elimu ya biashara wanawake kukabiliana na swala zima la uchumi ikiwemo na kuachana na anasa ambalo ndio kubwa ametuusia Mbunge wetu Zungu” amesema.

Diwani Kata Gerezani  Bi. Fatuma Abubakar wa pili kutoka kushoto

Naye Afisa Maendeleo Kata ya Gerezani Zaida Mligite amesema tayari kata hiyo imeshaanza kuwainua wanawake kiuchumi kwa kuwapa mikopo ya asilimia kumi makundi yote inayotolewa na Halmashauri ambapo tayari vikundi saba vimeshanufaika na vikundi vitano tayari wako katika marejesho ya mwishoni.

Baadhi ya wanawake wakiwemo mamalishe kutoka kata ya Gerezani wakifatilia uzinduzi huo


Chapisha Maoni

0 Maoni