SHEHE JALALA ALIA.NA AMANI NCHINI, AWATAKA WATANZANIA KUTOBAGUANAI

Shehe Hemed Jalala akizungumza katika ibada ya Krissmass kanisani hapo


Na Pilly Kigome

DAR ES SALAAM.

SHEKHE Mkuu wa Jumuiya ya Shia Ithna'ashariyyah Tanzania,Sheikh Hemedi Jalala ameungana na wakristo katika kuadhimisha sikukuu ya Krismass kwa lengo la kudumisha amani nchini.

Shehe Jalala ameungana na wakrtisto wa Kanisa la Golan Christian Church lililopo Kibamba Wilayani Ubungo jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwaunga mkono ikiwemo kuhubiri amani na upendo katika jamii ya watanzania.

Amewataka Watanzania kuendelea kuilinda na kuitunza tunu ya Amani, Umoja na mshikamano uliopo ili kuweza kuendelea kuwa na tunu hiyo pasipo kuweka matabaka ya udini.

Sheikh Jalala amesema kwa mujibu wa vitabu vyote vitakatifu Quran na Biblia vinaagiza kuwa na upendo pasipo ubaguzi wa rangi wala dini kwani kufanya hivyo kutadumisha amani ya kudumu pasipo magomvi na migogoro isiyo ya lazima.

Amebainisha nchi ya Tanzania Mwenyezi Mungu ameijalia amani ambayo wanaitengeneza wenyewe na kuasa tunu hiyo adhimu ni kuilinda isije wakaingia katika majanga akitolea mfano kama nchi ya Gaza ambayo chanzo ya yote yale ni kukosekana kwa upendo ndipo amani ikatoweka.

"Amani na upendo kati yetu ndio kila kitu na ndipo ilipo neema ya Mungu kwa waislam, wakristo na wasio na dini na ndio maana leo tumeweza kukutana pamoja na kusherekea sikukuu hii ya krismasi" Amefafanua

Naye Mratibu Taasisi Sambaza Upendo na Amani, Banza Ikomba ameviambia vyombo vya habari kuwa wao kazi yao kubwa ni kusambaza upendo na kuhubiri amani katika nyumba za ibada kwa dini zote ili amani isiweze kutoweka nchini.

Amesema taasisi yao iko katika majukumu mazito ya kutangaza amani na ndio sababu hata kiongozi huyo mkubwa wa dini ya kiislamu ameweza kufika kanisani hapo kujumuika pamoja hiyo imetokana na amani wanayohubiri.

"Tunatoa pongezi kwa kiongozi wa dini ya kiislam dhehebu la Shia,Sheikh Hemedi Jalala kwa kujumuika nasi katika ibada hii ya kuadhimisha sikuku ya kuzaliwa kwa Yesu kristo kitendo hiki ni cha faraja kubwa kwetu na kinaonyesha Upendo kati yetu kama watanzania,nasi tunajipanga kwenda katika msikiti wao pale Kigogo kwa wakati mwingine kuhubiri amani" Amesema Banda.

Mratibu wa Taasisi ya kusambaza Amani na Upendo Banza Ikomba akizungumza waumini kanisani hapo

Akizungumza katika tukio hilo Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Gogoni, Ally Arobaini ameushukuru uongozi wa kanisa hilo kwa kuwa na maono makubwa katika suala zima la amani kwa kuona kumkaribisha Shehe Jalala kwani waumini wamejifunza jambo kubwa sana.

Mbali na hilo amempongeza Mchungaji wa Kanisa hilo la Golan Christian Church Leonard Ntibanyike kwa maono yake makubwa na kuigusa jamii kwa kujitoa bila kuangalia maslahi yake binafsi na kusema ni mfano wakuiagwa katika jamii.

Baadhi ya waumini kutoka kanisani hapo wameiambia Nifahamishe kuwa wamefurahi na wamefarijika kwa kiasi kikubwa kwani viongozi hao wawili wa dini wameweza kutubadilisha kwa kiasi kiukubwa

Wamesema jambo kubwa walilojifunza ni kutokubagua kati ya mtu na mtu, dini na dini na hata kabila kwa kabila kwani kufanya hivyo amani nchini humu itadumu milele na milele.

Baadhi ya waumini wa Kanisa la Golan Christian Church wakifatilia ibada kanisa hapo


Chapisha Maoni

0 Maoni