Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dk Said Mohamed alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini.
DAR ES SALAAM
Na Mwandishi Wetu
JUMLA ya watahiniwa
572,338 wanatarajiwa kuanza kufanya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne kuanzia
kesho Novemba 13 hadi Novemba 30, 2023 ambapo kati yao 543,386 ni wa mashule na
watahiniwa wa kujitegemea ni 28,952.
Dkt. Mohamed amesema
katika watahaniwa wa shule 543,386 waliosajiliwa wavulana ni 250,237 sawa na
asilimia 46.05 na wasichana ni 293,149 sawa na asilimia 53.95.
“Aidha watainiwa wa
shule wenye mahitaji maalum ni 614 ambapo kati yao 283 ni wenye uoni hafifu, 24
ni wasioona, 135 wenye ulemavu wa kusikia, 11 ni wenye ulemavu wa akili na 161
ni wenye ulemavu wa viungo vya mwili,”amesema Katibu huyo.
Hata hivyo, ameeleza
kuwa kwa mwaka 2022 jumla ya watahiniwa wa shule waliosajiliwa walikuwa 534,753
hivyo kuna ongezeko la jumla ya watahiniwa 8633 sawa na asilimia 1.61 kwa mwaka
2023 ukilinganisha na mwaka 2022.
Watahiniwa wa
kujitegemea 28,952 walisajiliwa kati yao wavulana ni 11,867 sawa na asilimia
40.99 na wasichana ni 17,085 sawa na asilimia 59.01.
Amebainisha kati yao wenye
mahitaji maalum kwa wanaafunzi wa kujitegemea wakiwa nane kati yao wenye uoni
hafifu ni wanne na wasioona wanne.
Akielezea kuhusu
maandalizi ya mtihani, Dk Mohamed amesema yamekamilika ikiwa ni pamoja na
kusambazwa kwa mitihani ,vijitabu vya kujibia na nyaraka zote muhimu zinazohusu
mitihani husika katika mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar.
Aidha Katibu huyo
ametoa wito kwa kamati za mitihani za mikoa na Halmashauri kuhakikisha usalama
wa vituo vya mitihani unaimarishwa na vinatumika kwa mujibu wa mwongozo
uliotolewa na Baraza.
“Kwa upande
wa wasimammizi walioteuliwa kusimamia mtihani wahakikishe
wanafanya kazi yao ya usimamizi kwa umakini na uadilifu wa hali ya
juu,”amesema.
Kwa upande wa
watahiniwa, Baraza hilo limewataka kufanya mitihani kwa kuzingatia kanuni za
mitihani na kueleza kuwa halitarajii kuona mtahiniwa yoyote kujihusisha na
vitendo vya udanganyifu.
“Mtahiniwa yoyote
atakayebainika kufanya udanganyifu, matokeo yake yatafutwa kwa mujibu wa kanuni
za mtihani,”amesisitiza Katibu huyo.
Kwa upande wa wamiliki
wa shule na wakuu wa shule, Dk Mohamed amesema kwa namna yoyote hawatakiwi
kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mtihani katika kipindi chote cha ufanyikaji
mtihani huo.
Amesema baraza
halitasita kukifuta kituo chochote cha mtihani endapo litajiridhisha pasipo
shaka kuwa uwepo wake unahatarisha usalama wa mtihani.
“Aidha wakuu wa shule
wahakikishe wanatekeleza majukumu yao ya usimamizi kwa kuzingatia mwongozo wa
usimamizi ukiotolewa na Baraza na kuepeuka kuingilia usimamizi wa watahiniwa
ndani ya vyumba vya mitihani,”amesema.
Pia baraza hilo
limetoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano unaotakiwa kuhakikisha mtihani
wa kidato cha nne na maarifa 2023 unafanyika kwa amani na utulivu.
“Wananchi wanaombwa
kuhakikisha kuwa hakuna mtu yoyote asiyehusika na mtihani anaingia kwenye
maeneo ya shule katika kipindi chote cha mtihani kwani kwa kufanya hivyo tunawezesha
wanafunzi kufanya mtihanni kwa amani na utulivu,”amesema

0 Maoni