Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wanawake na Makundi Maalum,Doroth Gwajima
DODOMA
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Maendeleo ya
Jamii , Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Dkt.Dorothy Gwajima ametoa wito kwa
waajiri wa Maafisa Maendeleo ya Jamii kwenye Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka
za Serikali za Mitaa, Serikali Kuu, Mashirika ya Umma, Taasisi za Elimu, Mashirika
Yasiyo ya Kiserikali na Taasisi nyingine zote kuwawezesha wataalamu hao
kushiriki kongamano la wataalamu wa Maendeleo ya Jamii 2023.
Kongamano hilo litafanyika Novemba 20 hadi 22
mwaka huu na litakwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 60 ya Chuo cha
Maendeleo ya Jamii Tengeru likitarajiwa kushirikisha jumla ya washiriki 1500
kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Watakaoshiriki kongamano
wakiwemo kutoka Sekretarieti na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Serikali Kuu,
Mamlaka mbalimbali za Serikali, Vyuo na Taasisi za elimu ya Juu Mashirikia
yasiyo ya Kiserikali, Mashirika ya kimataifa, Mashirika ya dini, Mabonde ya
Maji, Majeshi, Taasisi za kifedha na Sekta binafsi.
Akizungumza na Waandishi wa habari kuelekea
Kongamano hilo leo Novemba 6,2023 Jijini Dodoma Dkt.Gwajima amesema ada ya
ushiriki shilingi laki tatu na elfu hamsini 350,000/=.
"Nitoe rai kwa waajiri wa Maafisa Maendeleo
ya Jamii kwenye Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Serikali
Kuu, Mashirika ya Umma, Taasisi za Elimu, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na
Taasisi nyingine zote kuwawezesha wataalamu hao kushiriki kongamano la
wataalamu wa Maendeleo ya Jamii 2023.,"amesema Gwajima
Dkt.Gwajima amesema, lengo kuu la kongamano ni
kutoa fursa ya wataalamu kujadiliana juu ya mchango wa sekta ya maendeleo ya
jamii na changamoto kwenye maendeleo ya taifa pamoja na kuendelea kubuni mbinu
za kutekeleza mipango ya Serikali ya awamu ya sita katika kuwezesha wananchi kujiletea
maendeleo endelevu kwa kutumia rasilimali zinazowazunguka. Kaulimbiu ya
kongamano hili ni “Sekta ya Maendeleo ya Jamii: Msingi Imara wa Uwezeshaji wa
Wananchi.”
"Kulekea maadhimisho hayo, shughuli
mbalimbali zinatarajiwa kufanyika kama vile; Mkutano Mkuu wa Maafisa Maendeleo
ya Jamii kutoka Sekretarieti na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mkutano wa Chama
cha Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii, Maonesho ya shughuli za Maendeleo ya
Jamii, Maonesho ya Taasisi na Vyuo vinavyotoa fani ya Maendeleo ya Jamii na
Mijadala ya kitaaluma,"
Na kuongeza kuwa "shughuli nyingine muhimu
itakayofanyika katika kilele cha maadhiimisho ya miaka 60 ya Taasisi ya
Maendeleo ya Jamii Tengeru ni uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa bweni la wasichana
( Girls' Hostel) lenye uwezo wa kulaza wanafunzi 568 na kumbi pacha za
mihadhara ( twin lecture theatre) yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1008 kwa
pamoja. Mradi huu uliogharimu shilingi bilioni 4.8 zilizotolewa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan umekamilika
na tayari umeanza kutumika," ameeleza Gwajima

0 Maoni