TMA YATHAMINI MCHANGO WA WANAHABARI KWA KUTOA TUZO 2023

 


Dar es Salaam;
Mamlaka ya hali ya hewa nchini TMA imesema inatambua mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika kutoa taarifa sahihi na kwa wakati juu ya hali ya hewa kwa wananchi.

Hayo yalisemwa na mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Bodi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Buruhani Nyenzi wakati wa hafla ya utoaji tuzo ya mwanahabari bora wa habari za hali ya hewa kwa mwaka 2023, iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Biashara (CBE), Dar es Salaam, Tarehe 30 Oktoba 2023.

"Ni furaha kubwa kuungana nanyi katika utoaji wa Tuzo mbalimbali ambazo ni ishara ya kutambua na kuthamini mchango na mafanikio yenu katika utoaji wa habari na taarifa za hali ya hewa kwa Jamii”. Alisema Dkt. Nyenzi.

Alisema kwa kutambua mchango wao mamlaka hiyo imekuwa ikitoa tuzo kwa waandishi wa habari kila mwaka ambao wamekuwa wakitangaza na kuchaputa taarifa za hali ya hewa nchini kwa lengo la kuongeza hamasa na kutambua mchango wao. 

Alitangaza majina ya washindi wa tuzo za mwaka huu ambapo mshindi wa tuzo ya jumla ni Bw. Mussa Kharid kutoka Kiss FM, mshindi wa upande wa magazeti alikuwa Bi. Pamela Chilongola kutoka gazeti la Mwananchi na mshindi wa upande wa mitandao ya kijamii alikuwa Noel Rukanuga kutoka Uhondo TV. 

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC) Dkt. Ladislaus Chang’a aliwaeleza wanahabari kuwa Mamlaka itaendelea kuboresha na kupanua wigo wa Tuzo za Wanahabari Bora wa taarifa za hali ya hewa na mabadiliko ya tabianchi kadri inavyowezekana, na aliwaomba wanahabari watoe maoni na mapendekezo ya namna bora ya kupanua wigo wa utoaji Tuzo ili kuendelea kuchagiza mwamko na umahili katika kutoa elimu na kusambaza tarifa za hali ya hewa.

Chapisha Maoni

0 Maoni