Wakala wa Usajili wa Biashara na
Leseni (BRELA), imeelekezwa kuwalea wafanyabiashara nchini kwa
kurahisisha jinsi ya kuifikia, kuwa mbunifu wa namna ya kuwahudumia na
kuifanya Taasisi kuwa ya watanzania ili kufikia malengo ya uanzishwaji
wake.
Maelekezo
hayo yametolewa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu
Kijaji alipokuwa akifungua mkutano wa kwanza wa BRELA na wadau wake leo
tarehe 27 Oktoba, 2023 kwenye ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es
Salaam.
Mhe. Dkt. Kijaji ameeleza kuwa, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
ameamua kukabidhi uchumi wa taifa kwa sekta binafsi na amefungua mipaka
yote, hivyo taasisi ya kwanza inayoshughulikia sekta binafsi ni BRELA
kwakuwa uchumi wa nchi unakua kupitia ukuaji wa sekta ya viwanda na
biashara nchini.
Ameongeza kwa kusema kuwa
kuanzia mwaka 2019 hadi Juni, 2023 Serikali imeeendelea kutekeleza
mpango wa kuboresha mazingira bora ya biashara na kuondoa tozo na kodi
mbalimbali zaidi ya 374 zilizosumbua wafanyabiashara ambapo Serikali
imefikia zaidi ya asilimia 75 ya dhamira yake.
“Kwa
mwaka wa fedha 2023/2024 kupitia Sheria ya Fedha jumla ya Sheria na
Kanuni 13 na pia Sheria ya Fedha ya mwaka 2023 zimeweza kupunguza na
kufuta tozo, ada na faini 67 ikiwa na lengo la Serikali ya awamu ya sita
la kuhakikisha mazingira ya biashara kuwa bora zaidi”, ameeleza Mhe.
Dkt. Kijaji.
Mhe. Dkt Kijaji amesisitiza kuwa
hakuna uchumi wa nchi unaokua kama hakuna maendeleo katika sekta ya
viwanda na ya biashara iliyo imara, Serikali inahakikisha inaboresha
mazingira ya ufanyaji biashara ndani na nje ya Tanzania na taasisi za
udhibiti hazitumii mamlaka zao kufungia biashara yoyote lengo ni
kuhakikisha kuwa sekta ya biashara inalea uchumi wa nchi.

0 Maoni